top of page

Spika azitaka PAC, LAAC na PIC Kumpa ushurikiano CAG Kichere


Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai amewaasa wajumbe wa Kamati za Bunge za Usimamizi za PAC, PIC na LAAC kumpa ushirikiano wa kutosha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliyeteuliwa hivi karibuni Bw. Charles Kichere


Ndugai aliyasema hayo katika ufunguzi wa mafunzo ya Uwajibikaji na Uwazi katika mikataba ya manunuzi ya umma kwa Kamati hizo za Usimamizi za Bunge yaliyoandaliwa na WAJIBU Institute of Public Accountability na kufanyika Novemba 9, 2019 katika hoteli ya Royal Village Jijini Dodoma.


“Uteuzi huu unakuja kama ukurasa mpya wa uhusiano kwetu sisi na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali” alisema Spika na kuongeza kuwa “Kichere ni mtu ninayemfahamu vizuri, naamini ana nia njema na tutafanya nae kazi kwa weledi.. naombeni tumpokee na tumpe ushirikianowa kutosha” alisema Mhe.Spika Ndugai.


Spika Ndugai aliishikuru taasisi ya WAJIBU chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji Ludovick Utouh ambaye ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mstaafu kwa kuandaa mafunzo hayo kwa wajumbe wa kamati hizo za Bunge za Usimamizi.


Akiongea kuhusu manunuzi ya umma, Spika Ndugai alisema “Katika masuala kama mipango na uzalishaji, mchakato wa manunuzi haukwepeki, naamni kupitia mafunzo haya mtaongeza uelewa katika mambo ya manunuzi na itasaidia katika kusimamia vizuri sekta ya umma” alisema Mhe. Ndugai.

Aidha, Mhe. Ndugai alipendekeza maboresho katika udhibiti na ukaguzi wa hesabu za Serikali huku akisisitiza suala la upokeaji wa taarifa kwa muda muafaka na kuongeza nguvu katika upande wa udhibiti wa rasilimali za umma.

“Bunge linatakiwa kujishughulisha na masuala wakati huohuo yakiwa bado ya moto moto, hivyo tunatakiwa kuangalia namna ambavyo tunaweza kufikia mduara wa matumizi ya umma ili tusipitwe” alisema Mhe. Ndugai.


Kwa upande mwingine Spika Ndugai alisema kwamba Ofisi ya CAG na Bunge zinaweza kwa kiasi kikubwa kufanikiwa katika upande wa ukaguzi wa hesabu za serikali lakini katika upande wa udhibiti kukawa na tatizo.


“Katika mfumo wetu, kipengele cha udhibiti hakijakaa sawasawa na ili tuweze kukitekeleza ni lazima yajengeke mazingira ya kikatiba yatakayoruhusu ofisi zetu hizi kufanya hivyo” aliongeza Spika Job Ndugai.


Wakati huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Nghenjwa Kaboyokwa alisema kuwa mafunzo hayo yana manufaa makubwa kwa Kamati za Bunge za Usimamizi kwasababu yatawawezesha kutekeleza jukumu lao la kuisimamia Serikali vizuri.


“Kama mnavyofahamu mabadiliko ya wajumbe katika kamati hizi yanatokea kila baada ya miaka miwili na nusu, hivyo mafunzo haya yanawasaidia wajumbe wapya kupata maarifa na uzoefu katika eneo hili la usimamizi wa Serikali” alisema Mhe. Kaboyoka.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa WAJIBU Ndugu Ludovick Utouh alisema kuwa baadhi ya mada zilizowasilishwa katika mafunzo hayo ni uwazi na uwajibikaji kwenye sharia ya manunuzi yam waka 2011, dhana ya mikataba ya manunuzi ya wazi, ripoti ya uwajibikaji ya viashiria vya rushwa katika sekta ya umma na mbinu za medani katika kuendesha mahojiano katika manunuzi kwenye sekta ya umma.



Featured Posts
Recent Posts
Archive
Search By Tags
No tags yet.
Follow Us
  • Facebook Basic Square
  • Twitter Basic Square
  • Google+ Basic Square
bottom of page